Watoto

“Mlee mtoto katika njia ipasayo naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.”

Lengo Kuu

Maono ya idara ya watoto yana msingi katika kitabu cha Mithali 22:6, “Mlee mtoto katika njia ipasayo naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.”
Hivyo basi idara ya watoto imelenga kuwafanya watoto wamjue Mungu na njia zake mapema iwezekanavyo.

Mgawanyo wa Miaka

Kundi la mwaka 3 hadi miaka 5, ni kundi  linaloitwa darasa la utukufu. Kundi hili linazingatia zaidi kuwahudumia watoto wadogo, kuwasimulia hadithi za watu maarufu katika Biblia. Panapo na nyenzo na vifaa, watoto hawa huonyeshwa katuni za Kikristo, hii inasaidia kumjua Mungu katika umri wa mapema katika maisha yao. Tunaomba watoto chini ya miaka 3 wabaki na wazazi maana wanakuwa hawana utulivu darasani.

Kundi la miaka 5 hadi 8, ni kundi  linaloitwa darasa la watakatifu. Kundi hili linazingatia zaidi juu ya watu mbalimbali maarufu wa siku za Biblia na mambo tunayoweza kujifunza kutoka katika hadithi zao. Pia watoto wanajifunza nyimbo za Kikristo na kukariri maandiko, wanawekewa mkazo katika kuikuza tabia ya Mkristo aliyeokoka. Michezo huweza kutumika kuwapa watoto wepesi kuelewa somo.

Kundi la miaka 9 hadi 12, ni kundi  linaloitwa darasa la nyumba ya mfinyanzi. Kundi hili linaweka mkazo zaidi katika kukariri maandiko na kupanda tabia za wokovu ndani ya watoto. Linaitwa darasa la nyumba ya mfinyanzi kwa sababu kuna tabia zinazoanza kuumbika kwa watoto hawa, hivyo ni muhimu kuwapa uzingativu kwani sasa wanaingia katika umri wa kupambanua mema na mabaya.

"Ni vema izingatiwe kwamba idara ya watoto si idara iliyokusudiwa kuwazubaisha watoto wakati wazazi wao wakiabudu, bali ni mahali ambapo yaliyo na thamani na maisha ya Kiroho yanapandwa katika maisha ya watoto hawa."

Makusudi ya Idara ya Watoto

  • Kuwafanya watoto wamjue Mungu kupitia njia za kupendeza, kuburudisha, na mazingira rafiki
  • Kuwasaidia watoto kujua watu muhimu katika Biblia na hadithi zao
  • Kuwafundisha nyimbo nzuri za Kikristo ili kuwasaidia kupenda Kanisa na kumpenda Yesu
  • Kuwafundisha tabia na mwenendo wa Mkristo kupitia michezo na ubunifu katika mafunzo
  • Kuwasaidia kukariri maandiko na kuwafundisha jinsi ya kutumia neno la Mungu kwa kulihifadhi mioyoni mwao

Siku ya Watoto Kitaifa

Jumapili ya pili ya mwezi wa Aprili

Ushuhuda wa Idara

kutoka kuwa mwanafunzi hadi kuwa mwalimu

 

 

“Namshukuru Mungu kwa malezi niliyopata kupitia idara ya watoto. Katika idara hii nimejifunza Neno la Mungu ambalo limeniongoza katika maisha yangu na katika nyanja tofauti, hata pale nilipokuwa pastor shuleni kwetu. Nimejifunza nidhamu na kuwa mnyenyekevu hasa katika kuhudumia wengine ambao nilikuwa na tofauti nao, hata kufikia kupigana mashuleni. Katika changamoto za makuzi nilizopitia, nakumbuka kufaulu na kufanikiwa kwa uwezo wa Mungu tu, wala si kwa uwezo wala maarifa yangu.” – Elia