Askofu Wetu
Askofu Dk. Manasse Daniel Martin ni mchungaji mwenye huduma ya kinabii, mshauri, mhubiri na mwalimu katika Neno la Mungu.
Dk. Manasse ni mzaliwa wa mji wa Mpwapwa, Dodoma. Alimpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake alipokuwa na umri wa miaka kumi na tisa.
Ni muhitimu wa elimu ya Theolojia katika ngazi ya Diploma toka chuo cha Elim Bible College cha Tanga, Tanzania, 1995. Kadhalika, amehitimu mafunzo ya elimu ya juu ya Uongozi na Huduma, yaani Restoration Theology, katika ngazi ya Shahada (Bachelor of Arts) toka Beacon University, Eldoret Rift Valley province, Kenya. Bishop Manasse ana shahada ya uzamili (master’s degree) na uzamivu (PhD) ya Systematic Theology and Ministry toka New Life Seminary, Virginia, Amerika.
Dk. Manasse amebarikiwa kuwa na mke mmoja, Ididi. Wamebarikiwa kuwa na watoto wawili, Tabitha na Samweli. Na wengine wengi wa kuwalea. Dk. Manasse ni Askofu mwandamizi (presiding Bishop) Elim New Covenant Church Tanzania (ENCC–Tanzania). Kadhalika, Dk. Manasse anahudumu kama mchungaji wetu mkuu wa ENCC–Mji wa Bwana.
Pamoja na kuwako katika utumishi kwa muda mrefu, ilikuwa ni tarehe 17 Desemba, 2004 Manasse D.M. aliposikia sauti ya Mungu yenye agizo lenye umuhimu na uzito wa pekee.
“Enenda kwa uwezo wako huu, ukakomeshe machozi katika nyuso za watu wangu. Je, si mimi niliyekutuma? Nitagusa pale utakapogusa na katika kinywa chako nimeweka uweza na kwa uweza huu utakomesha machozi katika nyuso za watu wangu.” – Waamuzi 6:14.
Hii ni sauti ya agizo la Mungu katika msingi wa kuwako kwa huduma ya Bishop Dk. Manasse D.M. Hii hupelekea, yeye pamoja na watumishi wote wa ENCC, kutumia vema kila fursa inayopatikana kuwafikia walio wengi – ikiwa ni fursa ya kifedha, machapisho, kanda (DVDs na CDs), vitabu, redio, TV, mitandao ya kijamii, n.k.
Kicho chake mbele za Mungu ni jambo la kwanza la msingi.