Abigaili
Abigaili

Ni idara ya wanawake ndani ya Kanisa la Elim New Covenant Church (ENCC) Tanzania. Maarufu ikifahamika kama Binti Abigaili. Idara hii inalenga kuwaunganisha wanawake wote katika kumtumikia Mungu katika huduma mbalimbali kanisani – Zaburi 68:11, “…wanawake watangazao ni jeshi kubwa”.

Idara hii inazidi kuwa baraka makanisani na hata majumbani. Kupitia idara hii wanawake wanapata kujifunza wajibu wao na kuwa wanawake bora ndani ya kanisa na katika familia zao. – Kutoka 35:25, “Na wanawake waliokuwa na mioyo ya hekima…”.

Ili kuendeleza idara wa wanawake wa ENCC Tanzania na kuleta mafanikio zaidi, Askofu Mkuu, Dr. Manasse D.M, alielekeza kuandikwe mwongozo utakaoiwezesha idara ya wanawake kutekeleza utumishi huu na kufanya kazi pamoja kwa kufuata taratibu zilizowekwa, zikilindwa na kuheshimiwa kwa kuiongoza idara.

KAULI MBIU YA BINTI ABIGAILI NI:

“Abigaili Jina Moja, Nia Moja, Sauti Moja”

Historia Yetu

Historia ya idara ya wanawake ENCC Tanzania, haiwezi kukamilika pasipo kutambua nafasi ya wanawake katika kanisa na jamii. Historia ya ENCC Tanzania inaonyesha jinsi wanawake walivyotumiwa na Bwana tangu mapema mwa kanisa kuanzishwa. Mikutano ya awali ya wanawake ilifanyika mapema miaka ya 2015 katika mikutano iliyofanyika Chalinze. Wanawake hawakuanza mikutano yao kirahisi, hapo awali mikutano yao ilikumbwa na changamoto kadha wa kadha. Ashukuriwe Mungu kwamba Askofu Mkuu, Dr. Manasse, na watumishi wote waliwaunga mkono na mikutano ya wanawake ilipoimarishwa iliwabariki wanawake na waumini wengi katika kanisa na kutumiwa na Mungu kuwaleta watu wengi kwa Yesu.

Masomo na mafundisho mengi yaliyofundishwa katika mikutano hiyo ya awali iliwapa wanawake wengi nafasi ya kumtumikia Mungu ndani na nje ya kanisa. Mama mchungaji Muturi kutoka Kenya alisema kuwa walijawa na furaha kuwaona wanawake waliowafundisha miaka kadhaa iliyopita walivyojihusisha kwa sehemu kubwa katika mikutano ya wanawake iliyofanyika makanisani. Wakina mama kadhaa wametumiwa na Bwana kusimamia idara hii mpaka sasa katika ngazi ya Jimbo na Parishi. Bwana amekuwa akiwatumia tangu waliposikia wito wa kufundisha na kuhubiri neno la Mungu.

Kalenda ya Binti Abigaili

Mei: kwenda na mawindo kupokea baraka, ngazi ya Kitaifa
Julai: kwenda na mawindo kupokea baraka, ngazi ya Parishi/Kanisa
Oktoba: kutakuwa na Kongamano la Kitaifa la Binti Abigaili