Dirisha la Pumzi ya Mungu

Download the English Version: The Window of the Breath of God – 2025 Prophetic Utterances.pdf

 

Huu ni ufunuo wa neema—neema inayokuja mara tano.

Mwanzo 6:16, 8:6; Ayubu 32:8, 33:4

Matamshi ya Kiunabii na Bishop Dr. Manasse DM

Bwana ametangaza mwaka wa 2025 kuwa Mwaka wa Dirisha la Pumzi ya Mungu. Kwenye Dirisha hili la Pumzi ya Mungu kuna neema iliyofichika. Imefichika kwa vizazi vingi na imefichika kwa kizazi kilichotangulia. “Kutoka katikati ya kabila na jamii za watu, watu wataiona pumzi yangu—pumzi ambayo itadhihirisha majira ya Dirisha la Pumzi Yangu kufunguliwa,” asema Bwana.

Hili ni dirisha lile lililofunguliwa wakati wa safina ya Nuhu, na maisha mapya yakaanza kwa ajili ya vizazi vya wanadamu. Ni dirisha lililofunguliwa wakati wa Rahab, kahaba wa Yeriko, naye akaiponya familia yake yote. Ni dirisha lililofunguliwa nyakati za Danieli alipokuwa akiomba kuelekea Yerusalemu, na kila namna ya mabishano na hila za wenye hila katika taifa la Babeli ikakomeshwa.

Ni dirisha ambalo halikuruhusu kifo cha Eutiko, kijana aliyekaza kusikiliza Madhabahu ikinena chini ya mafuta ya Paulo mtume. Ingawa alianguka toka ghorofa ya tatu akafa—mauti haikuweza kummeza kwa sababu Paulo alimwangukia shingoni mwake, naye akarejelewa na uhai wake.

Lakini sasa nikaona lango jingine limefunguka, lango linaloachilia mambo ya namna zote mbili—ghadhabu na rehema na neema. Bwana akasema, “Mamlaka za giza zimetawala malango haya tangu vizazi na vizazi, na Lango la lango ndilo lango la uumbaji lenye mamlaka ya kutawala vyote, mbinguni na duniani, na majini chini ya dunia. Lango hilo limefunguliwa mwaka huu. Lango la malango limefunguliwa ili kuleta hukumu. Hukumu na haki za Bwana ziweze kutimilizwa na ziweze kutangazwa usoni pa nchi katika uumbaji wake wote.”

Kwa nini ni Dirisha la Pumzi ya Bwana?

Huu ni ufunuo wa neema. Hii ndiyo neema inayokuja mara tano. Dhoruba zitakuwako, magumu yatakuwako, lakini neema hii itakuvusha nawe utakuwa kama hujapita mahala pa magumu. Hii ni neema ambayo baba zenu hawakuijua kwa sababu ya kutokutii na kwa sababu ya kuabudu miungu wengine, miungu wa sanamu. Lakini sasa, asema Bwana, nimekuja ili nikutaarifu ya kwamba: “Toba yako ya kweli nimeipokea, na maombi ya moyo uliopondeka nimeyasikia.” Na sasa ndipo natangaza ya kwamba, “Dirishakitu ambacho siku zote hukaa kimefungwamajira ya mwaka huu limefunguliwa. Ni Dirisha la Pumzi ya Mungu.”

“Tega sikio lako, fumbua macho yako katazame, nawe upate kuona ya kwamba: ‘Ni pumzi Yangu itakayokupa nuru katikati ya giza, ufunuo katikati ya kuchanganyikiwa, na uzima katikati ya udhaifu, na itakayokufungulia hazina za kutamaniwa za mahala pa siri zilizofichwa machoni pa walio wengi.’ Hili ni Dirisha la Pumzi ya Mungu.”

Bwana anena: “Uwe mwangalifu, ukatazame sana kuishika sheria ya mbingu. Maana nimekuja kwa majirio maalum katika majira haya ili nipate kutikisa misingi na viti vya enzimisingi ya viti vya enzi vya falme za wanadamu. Hazina zitatikisika. Mifumo itatikisika na kutetema. Na tazama, hata vyombo vya nguvu vitatikiswa.”

Ufalme wa wanadamu unapotikisika ni ili kiti cha enzi cha Mungu kilicho mahala Patakatifu pa Mungu kipate kupewa nafasi ya kuwa na mafungamano na viti vya enzi vya mfumo wa wanadamu.

Bwana ananena, “Nataka wafungamanishe Kiti Changu cha Enzi na viti vyao vya enzi ili nikawabarikie. Kupitia Dirisha la Pumzi ya Mungu, nitawavuvia hekima mahala pa kazi na mahala pa biashara. Dirisha la Pumzi ya Mungu litatimiza ahadi Zangu za kiunabii katika ndoa, uzao, na hazina zilizotazamiwa.”

“Je, sikuwataarifu jinsi ya kulifungua? Je, sikuwapa funguo za kulifungua? Lakini sasa nimekujaNIMEKUJAili nipate kulifungua mwenyewe. Kwa maana huu ndio wakati na haya ndiyo majira ya Jina Langu kutukuzwa katika vizazi vya wanadamu kwa kutimizwa kwa ahadi Zangu. “Nimeachilia malaika walinzi na wangojezi kati yenu, nao watafungua kila malango yaliyofungwa kwa sababu Dirisha la Pumzi ya Mungu linaachilia kiwango kingine cha mema yaliyocheleweshwa.” Haleluyah! Haleluyah!

Ni kupitia Dirisha la Pumzi ya Mungu wanadamu hupokea suluhisho. Dirisha hili la Pumzi ya Mungu liliwapa Wasamaria pumziko kupitia wakoma wanne. Dirisha hili la Pumzi ya Mungu linafunguliwa na hao wanaosimama kinyumekama Washami walivyosimama kinyume cha Wasamariawatausikia mvumo nao watarudi katika kambi yao wenyewe.

Ni dirisha la neema ninalokupatia: dirisha hili ni nyenzo, na Roho Yangu ndiyo Pumzi. Roho Yangu siyo nyenzo, natumia nyenzo ya Roho ili nikutendee yaliyo mema kwa pumzi ya kinywa changu. Natumia nyenzo ya Roho kukutendea yaliyo mema:

  • Nikupatie yaliyo mema kwa kasi, kwa kasi ambayo hukuweza kuiendea.
  • Nikupatie yaliyo mema kwa thamani, kwa thamani ambayo hukustahili.

Huna haja ya kuwa na hofu yoyote ili kuyafanya hayo yote yawe yametekelezeka. Ni Dirisha la Pumzi ya Mungu. Mwenye ufahamu na apokee, na yeye aliyebeba moyo uliopondeka na apokee.”

Hivi ndivyo Dirisha la Pumzi ya Mungu linavyofunguliwa kwako tena, ili kusudi yale yote yanayohusu maisha yako, familia yako, watoto wako, kazi yako, na hatima yako yapate hakikisho la usalama.

 

KWA MTU MMOJA MMOJA

Kwa sababu ya mafuriko ya neema yaliyoachiliwa katika majira ya mwaka huu, Bwana anena, “Usiyatafute makosa, usitafute hatia, na usiziendee njia za ubatili, kwa maana Bwana atahukumu kwa upesi bila kukawia.”

Neema ya kuwakomboa wale wamchao kutoka mahala pa hila na mtego, neema hii imezidishwa sana kwa ajili ya wale wamchao.

Kutakuwa na kuponyoka toka katika kongwa la mauti lililo dhahiri. Kama ilivyokuwa kwa Eutiko, utakutana na mambo yaliyokusudia kuondoa uhai wako. Lakini kwa kuwa umeingia katika mwaka huu wa neema mara tano zaidi, Dirisha la Pumzi ya Mungu limefunguliwa kwa ajili yako; utaponyoka na kutoka salama.

Katika msimu huu, kutakuwako na ustawi na mafanikio makubwa na ya haraka ambayo hayalingani na juhudi au mkakati wako. Mungu atabarikia kazi zako kwa neema yake. Juhudi yako kidogo itakupa matunda makubwa yanayotosha kuleta maswali juu ya utendavyo na jinsi unavyofanikiwa, kwa maana matokeo yatakuwa zaidi ya matarajio ya kibinadamu.

Tunza kushika uaminifu kwa kila jambo la kuaminiwa. Tunza kushika uaminifu kwa Mungu wako, Kanisa, wenye mamlaka, na mwanadamu chini ya mbingu. Bwana ananena, “Sitaweza kuunga mkono jambo lolote lisilo la uaminifu. Tunza kila jambo linalohusu kuaminiwa.”

Mwaka huu, pambanua na kujiepusha na kila rafiki asiyekuwa rafiki. Pambanua na kujiepusha na kila namna ya rafiki asiyekuwa rafiki. Dirisha litafunguliwa, na Dirisha hili linapofunguliwa linakupatia wewe neema inayofungua hazina za kutamaniwa. Neema inayokutambulisha wewe katika malango yatakayofidia miaka uliopoteza. Neema itakayokutambulisha wewe mahala ambapo: hakutakuwako na kukemewa, hakutakuwako na hofu, na hakutakuwako na makabiliano ya baraka inayogombewa.

Bwana ananena, “Nakupa Dirisha la Neema, mwaka huu. Nakupa dirisha la neema ya kufurahia matunda ya mema. Matunda ya mema yaliyoko katika nchi. Nyayo za miguu yako zinapokanyaga, matunda ya mema ya nchi hiyo nimekupatia. Hakutakuwako na malango yatakayoweza kusimama kinyume nawe kukupinga. Wajapoinuka, wataanguka kwa ajili yako. Watakapokusanyika, watatawanywa kwa ajili yako.”

“Usiyatafute makosa, usitafute hatia, na usiziendee njia za ubatili, kwa maana Bwana atahukumu kwa upesi bila kukawia.”

KWA MJI WA BWANA

“Ndani yako wako wenye hekima, na ndani yako, wameonekana watu wenye roho ya ufahamu. Wameonekana watu wenye roho yenye ufahamu. Hawa ni watu walionitafuta kwa mioyo yao yote—kwa subira na kwa kujidhabihu katika kweli. Nami niliposema nalimtafuta mtu miongoni mwao, mtu yule aendae kwa moyo wa unyenyekevu, mwenye akili na roho ya ufahamu, mtu aendae kwa unyenyekevu ili nipate kuuponya mji—kati yako nilikuta watu kama hao. Mwaka huu, nitakutimizia ahadi hii kwa ajili ya watu wako, Mji wa Bwana.

Nitaachilia uvuvio wa pumzi Yangu juu yako, Mji wa Bwana. Utasimama na kuinuka kama bonde la mifupa mikavu na kama jeshi kubwa la kufungua na kukomboa mataifa. Mwaka huu, nitatangulia mbele yako:

  • Nitaondoa kila jiwe la kikwazo lizuilialo
  • Nitakupa mwendo wa wepesi
  • Na kila shauri la Ufalme litatimizwa

Tazama, naweka wasaidizi na msaada uliowekwa tayari kwa ajili yako, ili uweze kwenda kwa kasi na kuthibitisha kuinuka kwa nuru yako juu ya taifa na mataifa. Usihofu kwa hofu yoyote ya taarifa za mkakati wa shetani uliopangwa juu yako ili kukukwamisha au kukupunguzia mwendo, kwani hakuna moja wapo ya taarifa hii itakayofanikiwa.

Kelele za shangwe zitasikika tena, na hao wamtafutao Bwana watakuwa faraja ya kudumu katika maskani ya Mji wa Bwana. Ghala zao hazitakuwa zimetindikiwa, kwa kuwa neema itasheheni katika maisha yao.”

“Utasimama na kuinuka kama bonde la mifupa mikavu na kama jeshi kubwa la kufungua na kukomboa mataifa.”

KWA ENCC

“Hapo kwanza ulisikia tu, lakini sasa umeona; umeona kwa macho yako yale niliyokutendea. Hapo kwanza hukujua, lakini sasa ni dhahiri machoni pako. Nawe umejua vema ya kwamba: ‘Wewe si wazo la mwanadamu; ni matokeo ya tumbo la roho iliyokuzaa. Wewe si pando la mwanadamu; ni mche uliopandwa na kupendwa na Mungu wako.’

Jihadhari na watu:

  • Viziwi wa kiroho
  • Bubu wa kiroho
  • Vipofu wa kiroho

Hawa ni wale wenye macho lakini hawaoni, nao wana masikio lakini hawasikii. Hawako mbali kwa kuwa wako miongoni mwenu, wako katikati yako. Wanapoisikia sauti ya shangwe, hawapigi kelele za shangwe. Wanaposikia maombolezo, hawaombolezi. Ni kama bubu, ni kama kiziwi, na kama kipofu asiyehusika na chochote. Ingawa macho yao yanaona lakini ni viziwi na bubu wa kiroho. Jihadhari nao maana wako miongoni mwenu.

Tazama, naweka mundu mkononi mwako. Mundu huu si silaha ya vita, bali ni zana ya kupulia, kwa maana mataifa yako tayari kwa mavuno kwa ajili yako. Yalete ghalani kwa utukufu wangu. Nakupa neema ya kuhifadhi mawimbi ya utukufu wangu. Hautaipoteza neema hii wala kupishana na mawimbi ya utukufu wangu.

“Wewe si wazo la mwanadamu; ni matokeo ya tumbo la roho iliyokuzaa. Wewe si pando la mwanadamu; ni mche uliopandwa na kupendwa na Mungu wako.”

KWA TANZANIA

Hofu iko juu yako—hofu ya mwaka uitwao “mwaka wa uchaguzi.” Lakini Bwana ananena hivi juu yako:

  • Aliye na shamba na abebe jembe aende shambani akalime.
  • Aliye na shule na aende darasani akasome.
  • Aliye na ofisi na aende kazini.
  • Aliye na biashara na aongeze mtaji na akasaini mkataba mpya.

Kwa maana amani nikupayo ni zawadi wala si juhudi ya mwanadamu. Ni zawadi, wala si juhudi ya mwanadamu.”

“Tanzania, nitakuinua tena na kukurejeshea heshima ambayo kwayo ulijulikana katika mataifa yote. Narejesha sauti ya haki na sauti ya ukombozi ambayo kwayo ulijulikana sana kwa ukombozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika. Tanzania hukupaswa kuipoteza sauti hii. Nami ninapokurejeshea ni ili usimame kwa ukombozi wote—wa taifa na mataifa—kiroho, kiuchumi, na kiufahamu. Matokeo yako yataupendeza moyo wangu tena.

Na kwa habari ya yale yote yakupayo hofu, wafanyao ghasia wamekwisha mezwa katika ghasia yao wenyewe. Hakutakuwako na ghasia.

“Tanzania, nitakuinua tena na kukurejeshea heshima ambayo kwayo ulijulikana katika mataifa yote.”

KWA AFRIKA

Afrika, sauti ya ukombozi imesikika. Baragumu ya uponyaji toka katika Dirisha la Pumzi ya Mungu, imesikika.

“Kuna baragumu inayosikika katika ulimwengu wa roho. Kwa sura hii, sauti ya baragumu inapaswa kusikika katika lango la kusini, ili Afrika ikapokee uponyaji unaotoka kwa Mungu tena.”

 

KWA MATAIFA

Bwana ananena, “Mashariki itainuka tena dhidi ya Magharibi.” Kuinuka kwa Mashariki dhidi ya Magharibi si kwa sababu ya agenda ya Mashariki dhidi ya agenda ya Magharibi, bali kwa ajili ya Israeli. Hata hivyo, ile saa ya utungu na maombolezo kwa ajili ya Israeli haijawadia. Haijawadia! Haijawadia!

Kwa hivyo, kila namna ya kuinuka kwa Mashariki kutanyamaza kimya kama ilivyoinuka—mpaka ile saa ya utungu wa Israeli itakapowadia. Hapo ndipo Gogu wa Magogu atakapoinuka. Na kule kuinuka kwa Gogu wa Magogu kutamhimiza Yeye aliye Mfalme wa Amani, atakayekuja na kutawala tena chini ya mbingu.”

 

Haya ndiyo asemayo Bwana kwa ajili ya mtu mmoja mmoja, Mji wa Bwana, ENCC, Tanzania, Afrika, na mataifa.

Bwana Akubariki mno!

Unaweza kutazama ibada hii ya kipekee hapa: