LANGO la Malango Kufunguliwa
“Lango ndiye Yesu Bwana,
wote waingie kwake.
Lango! Lango la Mbinguni li wazi.”
Ufunuo 22:14-15; 3:7-8; Isaya 22:22; Zaburi 82
Matamshi ya Kiunabii na Bishop Dr. Manasse DM
HALELUYA! karibu katika mwaka wa LANGO LA MALANGO KUFUNGULIWA.
Bwana akafumbua macho yangu,
nami nikaona malango angani na malango juu ya uso wa nchi. Kisha nikaona lango jingine limefunguka toka Mbingu za mbingu. Kisha Bwana akaniambia, “Haya malango unayoyaona ndiyo malango yaliyotawala maisha ya wanadamu. Maisha ya wengi kabla ya nyakati za vizazi kuwako. Yametawala isivyo halali. Nao wanaoyatawala malango hayo sio walioyaumba, sio wanao yamiliki, lakini wanayatawala.”
Kwa mara ya kwanza ikaja kwa uzito moyoni mwangu kwamba, hata malango yaliyoko angani ambayo hizo mamlaka na wakuu wa giza wanayatawala – wao hawakuyaumba, hawana haki ya kuyatawala.
Lakini sasa nikaona lango jingine limefunguka, lango linaloachilia mambo ya namna zote mbili – ghadhabu na rehema na neema. Bwana akasema, “Mamlaka za giza zimetawala malango haya tangu vizazi na vizazi, na Lango la lango ndilo lango la uumbaji lenye mamlaka ya kutawala vyote, mbinguni na duniani, na majini chini ya dunia. Lango hilo limefunguliwa mwaka huu. Lango la malango limefunguliwa ili kuleta hukumu. Hukumu na haki za Bwana ziweze kutimilizwa na ziweze kutangazwa usoni pa nchi katika uumbaji wake wote.”
“Lango hili ndilo linalokupatia wewe ufunguo wa Daudi.”
Na hapa ndipo anaposema, “Lango hili ndilo linalokupatia wewe ufunguo wa Daudi.” Ndivyo ananenavyo, “Nakupa wewe mlango ulio wazi, wala hapana atakayeweza kuufunga. Lango limefunguliwa kwa ajili yako, Lango limefunguliwa kwa ajili ya wenye haki, Lango limefunguliwa kwa ajili ya watakatifu.”
Hazina zile za milele zilizozuiliwa na hazina zile za milele kuwafanya watu warejee mahala pa mti wa uzima, malango hayo yamefunguliwa tena kwa ajili ya wanadamu. Lango hili, kwa upande mwingine limefunguliwa ili kuleta hukumu katika malango. Wakati wako watakaoshuhudia rehema na neema kwa kiwango cha juu kabisa mwaka huu, wako wale watakao kinywea kikombe cha ghadhabu ya Mungu kwa kiwango cha juu kabisa mwaka huu.”
KWA MTU BINAFSI
Lango litakupatia uwezo wa kuendelea mbele bila vikwazo, utaendelea mbele na kwa kasi kwa sababu kutakuwa na kasi nyingine ya malango ya uovu. Malango ya uovu yamejipanga ili kuendelea mbele kwa kasi lakini Bwana ataifanya kasi yako iwe kasi iliyo zaidi ya malango ya yule muovu.
Lango litayafanya maisha yako kukupatia viwango vipya vya mamlaka ya kiroho kwa kuwa unapewa amri na mamlaka ya kuuendea mti wa uzima. Mti ule ambao ulizuiliwa kwa miaka mingi na kulindwa na makerubi na maserafi, kwamba pasiwepo anayeweza kuuendea – mti huu ndio kiwakilishi cha mema yote awezayo kuwa nayo mwanadamu. Mungu ananena, “Lango hili limefunguliwa ili likuletee mamlaka mpya ya kiroho kwa kiwango kingine.”
Wengi watapita katika Lango hili na kupewa pumziko lao. Watapita katika Lango hili, watapewa shuhuda zao. Watapita katika pumziko hili, watarejeshewa yale waliyopoteza. Kwa baadhi ya watu yale waliyopoteza kwa miaka mingi yatarejeshwa katika maisha yao. Kwa baadhi ya watu watapewa utambulisho ulio mpya na utambulisho ulio wazi utakaojulikana wazi kwamba hawa ni watu walioitwa kwa jina la Bwana – malango ya muovu hayatawateka nyara, malango ya muovu hayataweza kuwagusa.
“Lango hili limefunguliwa ili likuletee mamlaka mpya ya kiroho kwa kiwango kingine.“
Lango hili limefunguliwa, Lango hili limeletwa ili kukutana na malango usoni pa nchi ili jukumu lako la kiuungu – jukumu ambalo ndilo sababu ya wewe kuzaliwa – lipate kutimizwa kwa wepesi ndani ya Lango hili. Unaingia katika Lango hili ili utimiziwe jukumu lile la kiuungu.
Lango litawakubali baadhi na kuwakataa baadhi. Lango litawakataa wale wote wanaodhani kwa sifa na juhudi zao wenyewe wanastahili. Wanadhani ni kwa wadhifa kwa vile walivyonazo, vile watendavyo na koo na jamii walizotoka – wale wote wanaotaka kutumia hazina za Mungu kumfurahisha shetani – Lango litawakataa. Na wale watakaokataliwa na Lango, utajua dhahiri kuwa malango yamewateka na Lango la malango limekataa kuwatumikia.
Wale wote wanaokula katika meza za shetani nao wanataka kula Meza ya Bwana, Lango litawakataa. Hili ni Lango la malango na ni Lango lenye kunena kufunguliwa kwa salama ya maisha ya watu kama mlango wa siku ya pasaka – mlango wenye Damu ya Mwanakondoo Yesu. Ni lango kama lango la safina ya Nuhu ambayo Bwana mwenyewe ndiye anayefunga kuhakikisha kuwa walio wake wanakuwa salama bila kujali ni dhoruba za namna gani zinazowazingira. Hili ni lango la Msalaba ambalo kwalo, nyota za mbinguni zilianguka ili kupiga saluti kwake Yeye aliyeutoa uhai Wake kwa ajili yako – ambalo makaburi yalifunguka na kuwaachlia waliokuwa ndani yake. Ni Lango la kazi ya Msalaba.
KWAKO MJI WA BWANA
Jueni ya kwamba, kwa lango hili Bwana ameamuru amani – Shalom katika mlima huu. Bwana ameamuru amani – Shalom ya Mungu katika mlima huu. Shalom itakuwa katika nyumba hii na juu ya vyote mlivyo navyo. Shalom itazingira milango ya nyumba ya wote wanaomtafuta Bwana katika mlima huu.
Lile gombo la chuo lililoandikwa tangu miaka ya kale kwa ajili yako, limeachiliwa kwa ajili yenu. Kama ilivyoandika katika Zaburi 40:7, “Tazama nimekuja katika gombo la chuo lile nililoandikiwa.” – ndivyo Yesu alivyonena katika Marko 14:21. Katika yale uliyoandikwa, ndiyo utakayoyatimiza, yatakayokujilia. Gombo la yale yaliyoandikwa kabla ya milima ya kale kuwa, limeachiliwa kutoka katika malango ya kale, limeachiliwa juu yako Mji wa Bwana. Gombo lile linenalo utukufu wa mwisho wa nyumba ya Mungu ambao utakuwa mkuu sana kuliko utukufu wake wa kwanza, limeachiliwa juu yako. “Haya yatatendeka, nanyi mtajua ya kuwa nimeyatenda mapenzi yangu makamilifu – nanyi mtanitukuza.”
“Shalom ya Mungu katika mlima huu. Shalom itakuwa katika nyumba hii na juu ya vyote mlivyo navyo.”
Lango la mamlaka ya kiuungu limefunguliwa, nami nitateta nao wanaoteta nawe. Nami nitafanya mioyo yao kuyeyuka, wale wote wanaopanda fitina, wanaopanda hofu, wanaopanda mashaka juu ya walio wangu. Kwa kuwa wataniabudu, wataniandama bila ya mashaka yoyote – nao watanitukuza kwani watauona uaminifu wangu.
Maana katika mlima huu, nitawafanyia watu wote karamu ya vinono. Unono wa divai yenye kuponya na kuhifadhi mifupa ya watu, mifupa na maisha marefu ya watu. Katika mlima huu nitaharibu kabisa uso wa sitara – ule wenye kutia giza mashauri. Nami nitatowesha giza lilifunika mataifa, giza lililofunika mataifa. Machozi, mauti, na kukemewa hakutasikika tena juu ya watu wangu kati yenu. Tazama nakupa mlango ulio wazi, kwa mambo ya chumba cha siri za Mungu. Hatima za watu, taifa na mataifa zitakuwa hemani mwako. Hatima za watu, taifa na mataifa zitakuwa hemani mwako.
KWAKO ENCC
AMKA, AMKA, AMKA asema Bwana. ENCC, ufunguo umeachiliwa mikononi mwako. Ufunguo wa joho la mawimbi ya wakati wa mwisho – mawimbi ya utukufu wa Mungu, uwepo wa Mungu. Hupaswi kupoteza nafasi yako. Nimeifanya njia yako kuwa ya wepesi, nimeifanya njia yako kuwa ya wepesi kwani wewe ni wa thamani kwangu. Nakupa usemi na sauti yangu. Nakupa usemi na sauti yangu itasikika kwa mataifa kupitia wewe.
“Lango limefunguliwa kwa ajili yako ENCC, Nami nitakufanya kuwa mnara wa sifa kwa mataifa yote.” Asema BWANA
Huu si wakati wa wewe kuwa dhaifu ENCC. “Itie nguvu mikono yako, na upewe uwezo wa roho ya ufahamu, upewe uwezo wa roho ya ufahamu. Kamwe usianguke katika shimo la yale yote yanayoumeza utukufu wangu.”
Shimo la:
- kupenda pesa
- kuupenda ulimwengu
- kiburi cha uzima
- kupenda madaraka na tamaa ya majivuno machoni pa wanadamu.
Yatunze na kuyashika vema yale yaliyo sahihi
- kicho cha Bwana
- utakatifu kwa Bwana.
Yaandame yale ya kanuni za kumpa Mungu nafasi ya kwanza. Kwani kwa kila jambo ulitendalo, “Kamwe, mimi Bwana, sitachukua nafasi ya pili.”
“Lango limefunguliwa kwa ajili yako ENCC, nami nitakufanya kuwa mnara wa sifa kwa mataifa yote.”
KWA TANZANIA
Mara mbili Mungu amefumbua macho yangu, akanionesha mambo ambayo kinywa changu hakiwezi kuyanena kwa wepesi. Kinywa changu hakiwezi kuyanena kwa wepesi. Ananena nini?
“Angalia, Ee Bwana; maana mimi ni katika dhiki; mtima wangu umetaabika; moyo wangu umegeuka ndani yangu; maana nimeasi vibaya sana; huko nje upanga hufisha watu; nyumbani mna kama mauti.”
– Maombolezo 1:20
Tukiwa katika mfungo wetu wa siku 40, sura ya mstari huu ilikuja kwa tafsiri ya tukio ambalo Bwana alinionesha katika ulimwengu wa roho.
Nilimuona Mchungaji wetu, Amiasi. Na mimi nikiwa sielewi tulikuwa katika eneo gani lakini ni ndani ya Tanzania, ila sio Dar-es-Salaam. Ni kama nimempata agizo la kutekeleza jukumu, na ikawa harudi kwa wakati ambao nilitazamia awe amerudi. Nikatoka kona nilikokuwako ili nimfuate aliko – ili nijue kinachoendelea maana alipaswa kuwa ameleta majawabu kufikia muda huo. Nilipoenda nikakuta ana jukumu kubwa – watu wamechimba kaburi kubwa ambalo watu wengi wamepangwa kwa pamoja. Naye alikuwa miongoni mwa watu aliyekuwa akiwasaidia watu kuwafanya hao watu waweze kupangwa. Na aliponiona, alikuja akiwa na moyo uliofadhaika sana. Nikamuuliza, “Nini kimetokea na hao watu ni nani; na kwanini imetokea hivyo?”
Ndivyo alivyoniongoza kwenda mahala kuingia mahala kama pa nyumba. Hakusema usemi wowote. Nikamuuliza, “Begi nilalobebea vitu vyangu liko wapi?” Akalichukua toka mahala kwenye chumba akalileta. Nilipolishika, sikulifungua kutazama ndani, bali nilipapasa kwa juu kuhakikisha vitu vyangu kama diary na tablet vimo. Yeye hakuongea chochote.
Nikaona nyumba ile kuwa ina mlango kushoto na mlango kulia. Akiwa anatoka kama akiwahi jambo jingine, ndipo ile milango ikawa ikifungwa na huku ndani kukawa na giza. Na saa ile nikawa nimefadhaika kwa fadhaa kubwa nikiwaza, ‘Wale wanaozikwa ni kina nani? Na kwa nini wanazikwa kwa wingi wa namna ile? Je, kuna vita, ujambazi, au kuna nini?’
Alipotoka kwa mlango wa kushoto, nikamfuata kwa mlango huo wa kushoto. Kutazama kwa ng’ambo nyingine, kulikuwa na nyumba nyingine ambako nilielekea ili kuketi na kuanza kungoja nipate majawabu ya kile kinachoendelea kutokea. Na hapa ndipo mahala ambapo Mungu alianza kunena nami kuhusiana na Tanzania.”
Tanzania, ndivyo Bwana anavyonena, “Kuna upanga huko nje. Kuna upanga huko nje lakini ndani ya nyumba ile ambayo milango ikifungwa kunakuwa na giza – huko nako kuna mauti.” Asema Bwana, “Nalikupa wewe mababa waliojitoa kwa vyote kwa ajili yako.” Mungu akanipitisha kwa kuwaleta mababa wa taifa, wale wote wa kisiasa na wale wa kiroho. Na nilikuwa na wakati wa kukamatwa kwa uzito wa kutosha. Hawa ni mababa ambao hawakuwahi kuwa na tamaa ya mali – walijitoa kwa vyote walivyokuwa navyo kwa ajili ya nchi yao na kwa ajili ya watu wao.
Hatuwezi kunena habari za mababa zetu wa kiroho, kina Kulola, kina Mgweno – ambao mpaka wanaondoka duniani hawakuona fahari yoyote ya vitu vya duniani. Fahari yao ilikuwa ni kuona sisi watoto wao tukiinuka kwenda kuyatimiza makusudi ya Mungu. Ndivyo walivyokuwa hao mababa wa kisiasa, kina Nyerere – ambao mpaka sasa unapojitambu-lisha kuwa wewe ni Mtanzania, kwa pasipoti yako – anayetajwa ni Nyerere. Anayetajwa ni mtu ambaye hakulihujumu wala kuliibia taifa lake.
Bwana ananena, “Nalikupa mababa waliojitoa kwa yote. Hawa walikuwa zawadi yangu kwako – mababa wa kiroho na mababa waliokuwa viongozi mliowaona kama viongozi wa kisiasa.” Maisha yao ya kujidhabihu yalikuwa ndiyo siri pekee ya mamlaka yao. Kwanini walipokuwa wakisema, wanadamu wanasikiliza? Kwanini walipokuwa wakinena, watu walikuwa hawawapingi – hata katika udhaifu na makosa yao? Ni kwa sababu ya maisha yao ya kujidhabihu. Walitoa vyote, hawakuzuilia chochote, na hawakupungukiwa na chochote.
Lakini sasa wale walio madhabahuni, ee Tanzania, wanatamani wawe katika siasa na wale walio katika siasa wanatoa maelekezo madhabahu zifanye nini. “RUDI, RUDI, RUDI Tanzania.” asema Bwana. “RUDI katika misingi yako ambayo kwa hiyo, mvua ya neema itakunyeshea na mema hayataondoka juu yako.” Kwa kuwa Yeye anayetaka kukutetea ndiye anayeshikilia fungo za Lango la malango.
“Iko wapi? Iko wapi sauti ya wale wanaowatetea wasio na hatia? Iko wapi sauti ya wale wanaowatetea wasio na sauti? Iko wapi sauti yao wanaowatetea wale ambao wamemwaga machozi na sauti ya damu yao imenyamazishwa? Iko wapi sauti inayonena kwa ajili ya wale ambao wasiponenewa hawatasikika siku zote za maisha yao?
RUDI – nawe upewe utetezi wa Lango. Rudi katika njia na misingi yako ya awali nawe upewe utetezi wa Lango.”
Bwana anauliza tena juu yako, “Iko wapi sauti ya wale wanaonena mashauri yaliyo nyooka na kuelekeza yaliyo sahihi, sauti ya wale wanaonena mashauri yaliyo nyooka na kuelekeza yaliyo sahihi – sauti ya wale wanenao ambayo kila inenapo hao waisikiao watasema, “Amen, Haleluya. Hii ni ya haki. Hii ni sauti ya kweli na haipasi kwa awaye yote kupingana nayo.”? Sauti ya kulipa taifa hakikisho la amani na uthabiti wa kesho yao. Iko wapi mikono ya hao wanaojitoa kwa kweli kwa ajili ya wahitaji? Iko wapi miguu yao iliyokataa kuandama udhalimu? Iko wapi mioyo yao wale ambao watakaa sirini wakiwa na machozi na uchungu wa kweli kwa ajili ya taifa lao?
Haya ni maelekezo ya wale wanaoomba kwa ajili ya taifa hili. “Ombeni, simameni katika mnara wa kumngoja Bwana. Mwiteni Yeye aliye Bwana aliye na funguo za kufungua malango. Hata ikawe ya kwamba yale yote ya fumbo za kanuni za kiunabii katika majira haya yakatimizwe juu ya taifa hili, si kwa huzuni, bali kwa shuhuda ziletazo furaha. Ombeni kwa ajili ya watu wale ambao wanayauza maisha ya watu. Watu ambao, kwa ajili yao, wako tayari kutumia fedha, madaraka, kazi za madhabahu za kiganga na uchawi, na hila yoyote ya wanadamu.
Watu hao huweza kuwa mtu mmoja lakini kwa ajili ya mtu huyu, watu makumi elfu kwa maelfu wakataabika – wakapotea. Wakapotea kwa sababu ya hiari yao kumuandama au kwa sababu anawatendea madhara.”
Dunia imekutana na watu namna hii tena na tena – watu ambao kwa mtu mmoja, dunia ilipigana vita iliyo kuu. Watu ambao, kwa mtu mmoja, taifa lilipoteza mwelekeo kwa miaka mingi na mpaka leo halijapata mwelekeo wake. Kwa mtu mmoja, maelfu ya watu – ikiwa katika miji au vijiji – mtu huyu mmoja amegeuza kabisa mwelekeo wa maisha ya watu. “Lango limefunguka kwa ajili ya kuwajibu watu hao ambao wanauza roho na nafsi za watu.”
“Iko wapi sauti ya wale wanaonena mashauri yaliyo nyooka?”
Omba wewe uombaye, kwa ajili ya ngome zile za kidini na ngome zile za mila na jadi zenye kuuza maisha ya watu. Ngome za kidini na ngome za maisha ya mila na jadi. Hii ndiyo ngome pekee ambayo Lango la malango alipokuja duniani, aliikuta, naye alitatizwa – hakutatizwa na wengine, alitatizwa na watu waliotetea mapokeo yao. Hakutatizwa na wengine, alitatizwa na watu waliotetea dini zao. Hakuhukumiwa na wengine, alihukumiwa na makuhani waliosema, “Heri afe kuliko hekalu letu libomolewe. Heri auwawe kuliko Kaisari aje atuangamize.” Lango la malango limefunguliwa ili kujibu kila mila, utamaduni, mapokeo, na dini ambazo kwa hakika zinasimama ili kuipinga sauti Yake.
Kwa wale wote waombao, omba kwa kuwa Lango liko tayari kuvamia malango yote yanayovamia mioyo ya watu. Kuna malango yanayovamia mioyo ya watu na kubadilisha mielekeo ya mioyo ya watu. Haya ni malango ya media, kielimu na mifumo yake yote, kisiasa na mifumo yake yote, kisheria na mifumo yake yote, taasisi za fedha na mifumo yake yote. Haya ni malango yaliyoko si kwa bahati nasibu.
Ni malango yaliyokusudiwa kuwa malango yanayotawala mioyo ya watu. Na mioyo ya watu ikiwa imefungwa kwa giza la jinsi hii, yale yaliyo mashauri ya kweli hayataweza kusimama. Lango limefunguliwa. Tanzania, ipende kweli, ipokee kweli. Ipende kweli, ipokee kweli. Ipende, ikumbatie, ipokee – itakuponya, na Lango la malango litakubarikia na kuwa msaada wako vivyo.
KWA AFRIKA
Afya yako ni dhaifu. Maradhi yanakutaabisha. Nami nikaona katika roho, maradhi anayonena ni kama aina ya tetanus zilizoingia ndani ya mwili wa mtu na huyu mtu akawa anapata aina ya degedege – kama mtu anayepigwa na kifafa.
Na Bwana anasema kwamba, “Afya yako imekuwa dhaifu. Mashujaa wako hawapo tena, na wenye nguvu wako wameanguka katika uwanja wa vita. Na wale uliowategemea wametekwa nyara, Afrika. Huwezi kusimama mwenyewe, huwezi kusimama mwenyewe, Afrika. Lakini sasa, Lango la malango limefunguka kwa ajili yako.
Afrika, ikiwa utanitafuta uso, utaomba, utajinyenyekeza mbele yangu, Mimi, kupitia Lango la malango mwaka huu, nitakurehemu, nitakuponya, nitakusimamisha. Fua mavazi yako, takasa mikono yako, kataa uongo na roho zidanganyazo – andama iliyo kweli, niko tayari kukuponya.”
“Huwezi kusimama mwenyewe. Lakini sasa – Lango limefunguliwa.”
KWA MATAIFA
Lango la malango limefunguka. Kutakuwa na malango ya malango yaliyotaabisha mataifa, yakachukua mateka mataifa ya dunia. Mwaka huu yatakutana na hukumu ya Lango la malango. Kama ilivyokuwa katika Babeli ya kale, Bwana ananena, “MENE MENE TEKEL NA PERESI imeandikwa katika kuta zao.” Wataanguka wala wasiinuke tena. Anasema, “Nitapita kwa kisasi changu ili nilipe kisasi cha damu kwa wale wote waliomwaga damu isiyokuwa na hatia.”
Bwana anasema, “Nitawaruhusu kujiinua ili anguko lao liwe la wazi machoni pa wote. Nitaufutia mbali ukumbusho wao na njia zao hazitaonekana tena na kumbukumbu lao halitakuwako. Nitainua kizazi kipya cha watu watakaonitukuza.”
WEKA UZINGATIVU:
Weka uzingativu kwamba kuna roho zidanganyazo. Katika mwaka huu ndiyo nyakati ambazo nabii wa uongo anayetengeneza njia na mapito kwa ajili ya mpinga Kristo anaenda kujitambulisha na kutokea wazi kuliko nyakati na karne na milenia nyingine zozote zilizowahi kuwako. Na kwa sura hiyo, unachokihitaji ni neema ya Mungu ili kupambanua kweli inayotoka kwa Mungu – na hiyo ukaiandame.
Lango la malango limefunguliwa.
Nami niliona jambo moja katika ulimwengu wa roho. “Hili Lango la malango lilipofunguliwa, likaanza kuja likikaribia haya malango mengine. Na malango mengine yalipisha yakawa hayaonekani yako wapi. Na Lango la malango likaja hadi likakutana na nchi. Kwa hivyo wanaotoka katika nchi wanaweza kupenya kwenda kwenye Lango la malango. Na Lango hili la malango likawatendea yaliyo mema.
“Malango yale mengine yoyote yatafumba kinywa, Lango la malango na lipewe sauti katika maisha yako.”
Kwa mara nyingine tena: “HUU NI MWAKA WA LANGO LA MALANGO KUFUNGULIWA.”
“Lango la malango na lifunguliwe, na lifunguliwe, na lifunguliwe, na lifunguliwe. Kwa ajili yako lifunguliwe, kwa ajili ya walio wako lifunguliwe.”
Hii ndiyo sababu wimbo “Liko Lango Moja Wazi” umekuwa ukiimbwa sana ndani yangu. Hili ni Lango la Mbingu za mbingu. Hili ni Lango linapofunguliwa linaleta majawabu ya pande zote. Majawabu ya kuwakabili adui zako na majawabu ya kukutendea wewe yaliyo mema. “Mwaka huu Lango hili litafunguliwa.”