Mdhihirisho wa Mawimbi ya Utukufu wa Mungu

Habakuki 2:14

 Afrika: kwa nini?

Afrika hauna adui mwingine, kwa nini wewe ni adui yako mwenyewe? Afrika kwa miaka mingi na kwa karne nyingi wewe umekuwa ni adui yako mwenyewe. Ndiwe uliyeua watoto wako mwenyewe. Ardhi yako ikapokea damu ya uzao wako mwenyewe. Afrika, kwa nini? Afrika kwa nini umechagua kuwa adui yako mwenyewe? Kwa kuwa sasa ikiwa ulihitaji msaada, umesaidiwa na sasa hauna adui mwingine, ila wewe ni adui yako mwenyewe.

Mtazame Daudi wako Afrika. Hapa Daudi wako ananena kila kiti cha enzi, ananena kila mfalme aliye na taji kichwani. Ananena, “Mtazame Daudi wako anapoiacha agenda yangu na akakamatwa na moyo wa kumzingatia Absalom. Absalom ni mwana wa Daudi lakini Absalom ana agenda ya kumuua kila mtu katika taifa. Na yeye aliye katika kiti cha enzi amemkumbatia kwa sababu ni uzao wa kiuno chake.” Daudi, hivi ndivyo Bwana anavyonena, “Iko agenda ya Mungu juu yako Afrika, iko agenda ya Mungu juu ya taifa, iko agenda ya Mungu kwa vizazi vinavyofuata. Unapomtaka Absalom kuishi, Bwana atamuua Absalom na unapotaka Daudi wewe mwenyewe ufe, Bwana atamfanya Daudi kuishi.”

Mara hii ndipo Bwana akanena, “Nakutuma kama Kushi. Kushi sio nabii wa maangamivu, Kushi hatamani mabaya yawatokee wengine lakini mara hii anabeba ujumbe wa huzuni. Nae Kushi anapoelekea ananena habari ambayo itamfanya Daudi kutokwa na machozi. Na anayoyasema Daudi kinywani, yanaujaza moyo wa Daudi kwamba, “Heri mimi ningekufa, Absalom aishi”. Je, ni heri agenda ya Mungu ife, matakwa ya moyo wako yaishi? Daudi, ni heri agenda ya Mungu ife, ni heri kizazi kinachokuja kipotee na matakwa ya moyo wako yaishi?”

Mungu anasema, “Kwa hakika nitayaua yale unayotaka yaishi, nitayafanya yaishi yale unayotaka yafe. Nitayaua yale unayotaka yaishi, nitayafanya yaishi yale unayotaka yafe. Na hii itabaki ikijulikana katika vizazi vyenu vyote, ya kwamba shauri langu litasimama. Shauri langu litasimama. Shauri langu ndilo litakalosimama. Hii itabaki kuwa kumbukumbu kwa vizazi vyenu vyote.”

Afrika, kwa nini? Kwa nini kuikumbatia roho ya malkia wa Kushi? Yeye aliyeondoka ili aende safari akiwa amewekwa wakfu lakini hakujiweka wakfu kwa Mungu wa kweli. Aliondoka ili aende katika safari ya wanaoabudu lakini hakuwa miongoni mwa wanaohitaji ibada. Aliondoka ili aanze safari ya kwenda kama msafiri lakini hakuwa na safari ya mbingu. Aliondoka ili aende safari akiwa na hazina, lakini hakujiwekea hazina mbinguni. Aliondoka ili aende safari ya Jerusalem mahala pa Madhabahu, lakini hakuwa na moyo wa ibada.

Afrika, majira yamewadia. Unataka milango iliyo wazi? Majira yamewadia. Unataka kwenda mahala pa Madhabahu? Nipe moyo wako. Nipe moyo wako. Nipe moyo wako.

 

Tanzania: jawabu li ndani yako

Kwako wewe Tanzania. Kuna mambo unahitaji msaada utokao kwa Mungu kwa kila namna uwezavyo kumngoja katika mwaka huu. Naliona katika roho watu wawili. Watu wawili waliokuwa wanachukuliwa na upepo wa kimbuga. Mmoja amevaa mavazi meupe na mwingine amevaa mavazi ya kijani. Na Mungu akasema, “Watu hawa wawili wanawakilisha vyama viwili vya siasa vinavyoenda kukumbwa na kuchanganyikiwa kwa kiwango cha juu. Na unavyoona upepo wa kimbuga ukiwachukua wanaenda kwa kusamasoti (somersault), ni kwamba wanaenda bila ya control yao wenyewe. Kuna mambo unahitaji Madhabahu kumuita Mungu ili kuhakikisha kwamba maisha ya watu hayapotezi mwelekeo kwa sababu ya hali ya kuchanganyikiwa iliyo tayari kuwakumba watu kwa upepo wa kisulisuli unaochukua maisha ya watu hawa.”

Bwana akasema, “Unahitaji kuomba kwa ajili ya watu wenye majina maarufu na walio na nafasi za madaraka. Omba kwa ajili yao kwa sababu wengi wao hawajajua ya kwamba kuna shimo na mtego vinavyowangojea.”

“Tanzania, suala la uchumi halijawahi kuwa tatizo lako. Suala uchumi sio tatizo lako. Suala la uchumi halijawahi kuwa tatizo lako. Suala la uchumi si tatizo lako. Tatizo lako huna watu wakusimamia hazina nilizokupatia. Watu wenye moyo wa ukomavu; watu wasiolia kama watoto. Unahitaji kuomba Mungu ainue viongozi walio kama wazazi. Wazazi ambao hawatalia njaa wakati watoto wakilia njaa. Watakuwa na majawabu na wala wao hawatakimbilia mezani kwa sababu wanayo majawabu ya watoto wao. Unahitaji viongozi wakomavu, viongozi wenye moyo wa kweli – moyo wenye uchungu na thamani ya maisha ya watu na vizazi vijavyo. Suala la uchumi halijawahi kuwa tatizo lako na si tatizo lako. Hazina nilizokupatia zinatosha kuwa jawabu la kila swali linalokuja la uchumi wako.”

 

Kanisa: unahitaji kuvuka kwenda katika ng’ambo ya 2022

“Kwako wewe Kanisa. Yako yale ambayo wewe mwenyewe unayatarajia. Yako yale ambayo Mungu anayatarajia kwako, na yako yale watu wanayatarajia kwako. Yale unayoyahitaji si utukufu wa nyakati zilizopita, si utukufu wa miaka iliyopita. Unahitaji kuvuka kwenda katika ng’ambo ile. Na hatua za miguu yake zimeanza kukanyaga ng’ambo ile ya mwaka 2022 ambayo ilikuwa ahadi yangu kwako.”

Nyakati zozote unazoendelea mbele katika mwaka huu, epuka roho ya Balaamu. Epuka roho ya Balaamu. Epuka roho ya Balaamu. Hii ni roho inayojaribu kumshawishi Mungu atende yale ambayo Mungu keshasema “Hayo sitatenda!”. Hii ni roho inayomaanisha, Mungu amesema, “Huwezi kuwalaani watu hawa kwa sababu nimewabariki.” lakini ikaendelea kujenga madhabahu tena na tena ikifanya majaribio ya kuwalaani. Hii ni roho ya Balaamu: ya watu wanaoenenda katika njia zao wenyewe na katika matakwa yao wenyewe huku wakitamani Mungu kubarikia yale ambao wao wanayatamani nayo hayako katika agenda ya Mungu. Unataka kuuona utukufu Wake mwaka huu Kanisa, ondoka mahala pa roho ya Balaamu.

Unatakiwa kuondoka katika kila namna roho ya Lutu. Lutu ni mtu ambaye Mungu alimuandalia mlima wa agenda yake. Malaika wa Bwana walimwambia Lutu, “Kuna mlima aliokuandalia Mungu.”, naye akachagua kubaki katika bonde alilolitamani mwenyewe. Hakuamini habari ya malaika, hakuamini agenda ya Mungu, akakumbatia matakwa ya moyo wake na hatima yake Lutu hakuwa salama. Maana kwa binti zake wawili, alizalisha kizazi cha wana walio harama. Hawa ni wote walio wamoabi na wote walio waamori kwani hakwenda katika mlima wa agenda ya Mungu katika maisha yake.

Yakupasa kuondoka katika roho ya Tera. Kanisa, yakupasa kuondoka katika roho ya Tera. Tera ndiye baba yake Ibrahimu aliyeanza safari kutoka Uru ya Wakaldayo ili aende Kanaani naye akaishia Padan-aramu. Akakaa huko, Tera akafa. Tera alianza safari bila ya Mungu. Tera alianza safari akiwa hana Mungu. Kanisa, ondoka mahala pa roho ya Tera. Chochote unachojaribu kukitenda, Kanisa, hakikisha ya kwamba Mungu anaenda pamoja nawe. Kama wanafunzi wake walivyomchukua mashuani, mbebe pamoja nawe kutwa kuchwa, kutoka kwako na kuingia kwako.

“Dhoruba zitainuka katika safari lakini usiziogope dhoruba, niogope mimi. Usiiogope dhoruba, niogope mimi. Usiiogope dhoruba, niogope mimi Mungu ambaye nina uwezo wa kunena na dhoruba na dhoruba ikakaa kimya. Usiogope katikati ya dhoruba kwa sababu yale yote yanayokupa wewe hofu hayo hayatatendeka. Yale yote yanayokutisha hayo hayatatimia. Yale yote yaliyo hofu yako hayatakupata. Yale yote yaliyo hofu yako, hayatatendeka.”

Bwana anena ya kwamba, kuandamwa  kokote kwa yale yaliyokuwa yakiongeza huzuni, yote yaliyokuwa yakichochea moyo wa huzuni na maombolezo, vyanzo vya nguvu za hayo vimeuwawa na kung’olewa. Vimeuwawa na kung’olewa. Kwa kuwa kutokea miongoni mwetu Bwana ananena, “Farao yule uliyekimbia uso wake utasimama mbele yake nawe ukiwa umembeba Bwana, ukiwa na majawabu ya vizazi vingi vijavyo. Farao yule uliyemkimbia uso wake utasimama mbele yake tena. Haya ndiyo niliyokuandalia mbele yake kwa kuwa katika mwaka huu utakuwa na kuongezeka kwa ukubwa, kwa kina, kwa mapana, kwa ustawi, kwa kufurika. Fungu mara saba, fungu mara mia, fungu mara elfu, na fungu mara kumi elfu liko tayari kuachiliwa kwa ajili yako.”

“Shuhuda zile ambazo zitakuwa wazi, shuhuda ambazo hazitangoja uzielezee ili watu waone, shuhuda ambazo macho ya watu yatatazama yaone kuna jambo limekutokea – uwe tayari kuzipokea mwaka huu. Shuhuda zile zitakazofanya watu waje na wanyenyekee mbele zako ziko tayari kukutokea mwaka huu. Shuhuda zile zitakazofanya watu waliche jina la Bwana Mungu wako ziko tayari kukutokea mwaka huu. Shuhuda za yale yatakayofanya watu wamkubali Yesu ziko tayari kukutokea mwaka huu.

 

Kwako wewe kibinafsi: Bwana kasikia, kaona, kaja kufumbua mafumbo

“Kwako wewe kibinafsi. Umeningoja katika mlima huu. Nimesikia sauti ya kuomba kwako, nimeyaona machozi yako, nimetambua kuugua kwako, nimekuja ili niwe msaada wako. Nimekuja ili nikusaidie. Yale yaliyokuwa fumbo la miaka mingi tangu sasa hayatakuwa fumbo kwako tena. Neema ya mlango kuwa wazi itakayofumbua mafumbo yaliyoko juu ya uso wa nchi imeachiliwa mikononi mwako. Imeachiliwa mikononi mwako.”

“Uwe makini, uwe mwangalifu, weka uzingativu kwa kanuni zote za mbingu. Weka uzingativu wa kanuni zote za mbingu kwani kwa kuziandama na kuzifuata ndivyo unavyovikwa mamlaka na kutawala usoni pa nchi. Uwe mwangalifu, weka uzingativu kwa kuwa Mungu analitazama Neno lake ili aweze kulitenda. Mkono wako unaponyooshwa katika hazina zile za gizani ni kwa sababu Mungu amekupatia. Mkono wako utanyooshwa katika utajiri wa mataifa, mahala pa siri, mahala ambapo pamehifadhiwa kwa karne na kwa vizazi vingi. Sasa mkono wako utanyooshwa kwani Mungu amekupatia.”

Fumbua macho yako nawe ukaone. Fumbua macho yako nawe ukaone, ukatazame. Ukaone mlango wenye milango, mlango wenye milango umefunguliwa. Mlango wenye milango. Na MLANGO huu ni Yesu Kristo mwenyewe, ndani yake kuna milango ya safari itakayokufanya upewe shuhuda zako, upewe hadhi yako, upewe heshima yako, upewe wimbo wa kumtukuza.”

Haya asema BWANA.