Bwana Mungu wa Utukufu Amekaa Kitini pa Enzi – Zaburi 47:2

Maana kwa mara nyingine, vilio na maombi ya watu waombao usiku na mchana kutokea mahali hapa vimenijilia, vimenifikia, nami nimeshuka, nami nimekuja. Nami nimekuja nikiwa na ujira wangu kwa ajili ya wale walio wangu, wapewe yaliyo mema. Kwa ajili ya wale walio kinyume changu, nimekuja na ujira wa kisasi chao. Wale walio ngojea msaada wangu, watauona msaada wangu. Na wale walio tamani kutafuta msaada wa kila namna ya kazi za miungu wasiokuwa Mungu, mahala pao hapataonekana. Watu hawa watakataliwa, watakataliwa katika mamlaka, watakataliwa katika shughuli za uchumi, watakataliwa wale walio muinua mungu wa Misri; watakataliwa na kuondolewa katika mahala pa afya kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya. Wote waliojitenga mbali nami, wamejitenga mbali na amani yangu. Hawakujua wanachokitafuta, na rehema yangu iliyo nyingi iko tayari kuwatosheleza. Iko tayari kuwatosheleza. Hawa ni watu ambao wamekaza shingo zao na kufanya mioyo yao kuwa migumu. Kwao hakuna nuru, kwao hakuna mchana, wanaenda mchana wakipapasa kama kipofu apapasavyo nyakati za usiku.

Kanisa, umesikia ikinenenwa ya kwamba: “hukumu huanzia nyumbani mwa Mungu.” Naam, na ipite mbali nami, ipishe mbali nami kwamba Bwana Mungu wa dunia yote nisitende iliyo haki. Ipite mbali nami kwamba Bwana Mungu wa dunia yote nitende udhalimu, la hasha. Nimemtuma mjumbe wangu wa kuwafundisha, wa kuwahubiria, na kuwaelekeza njia inayowapasa kuiendea – njia inayowapasa kuiendea. Wengi wenu mmechagua kuisikiliza na kuiendea njia ile ya kidunia. Wengine wenu mmechagua kuwa na masikio yenye utafiti, masikio yanayowasha, yenye kusikiliza ili mpate kuchagua nini cha kutenda na nini cha kutokutenda. Wako wale walio wachache ambao wao wanampenda Mungu kwa hakika, lakini wamenaswa katika njia panda ambayo hawajui ni nini hasa kinawapasa kutenda na kwa njia gani inawapasa kuendea.

Lakini kwako wewe ambaye kwa kina na kwa moyo, ambaye umemfuata Yeye katika njia ya agano, haya ndiyo anenayo kwako: nitadhihirika kwako, nitadhihirisha Roho ya Umasihi wangu juu ya maisha yako – nitadhihirisha Roho ya Umasihi wangu juu ya maisha yako. Na kazi zile za Masihi, kama mlivyosikia habari za Yoshua wa zamani, ninakuja kwako kwa jina langu – Yeshua. Yeshua aliye Masihi ili nikuonyeshe wokovu wangu, nikuonyeshe wokovu wangu, nikuonyeshe wokovu wangu. Nitakukomboa kutoka mahala pa mkono wa adui. Nitaukomboa uhai wako kutoka mahala pa mateso na kila namna ya mguu wenye kukukanyaga ili kukutweza. Nikupatie nyara za mataifa kuwa urithi wako. Nitakuja kwa jina langu la maagano nikuonyeshe wokovu wangu kama Yeshua aliye Masihi.

Nitaruhusu uumbaji ukutumikie. Maana uumbaji utatimiza na kutekeleza yaliyo agenda yangu. Nitaachilia watu walio sahihi, watu walio sahihi watakaoandama yale yote yaliyo sahihi. Na wale wote wakupingao watapingwa. Wewe ambaye umeweka nia moyoni mwako, ukanena na moyo wako, haya ndiyo anenayo Bwana kwa ajili yako. Nitakuondolea ugonjwa kutoka katikati yako. Nitakupa nguvu, naam nguvu kama za nyati. Nguvu zitakazokupa kwenda umbali mrefu ukayatimize yale yote niliyo yaachilia juu yako kwa ajili ya mavuno ya siku hizi za mwisho. Nitakupa ushuhuda, nitakupa ushuhuda wa kibali. Yale yote ambayo hapo kwanza yalikupinga, yale yote ambayo hapo kwanza yalikataa kukutumikia, kibali kinakuja juu yako ili yakutumikie.

Kwa mara nyingine, neema ya kutengwa na mabaya inaachiliwa juu yako, neema ya kutengwa na mabaya inaachiliwa juu yako, neema ya kutengwa na mabaya inaachiliwa juu yako. Hakuna majanga yatakayo chukua utukufu wangu, hakuna majanga yatakayo chukua utukufu wangu. Nimekuja ili nichukue mahala pangu, ili niutetee utukufu wangu. Nimekuja ili nikae mahala ninapostahili, mahala pa kiti changu cha enzi. Ndivyo nitakavyouita mwaka huu: BWANA MUNGU WA UTUKUFU YUKO KITINI PA ENZI. ‘Bwana Mungu wa utukufu ameketi kitini pa enzi’, ndivyo mtakavyoukumbuka mwaka huu. Ndivyo mtakavyosemezana kila mmoja na mwingine, ‘Bwana Mungu wa utukufu amekaa kitini pa enzi’.

Kanisa, nakupa wewe nyenzo, nakupa wewe jina, nakupa wewe sauti. Sauti ambayo haiwezi kunyamazishwa. Maana ziko sauti zitakazoinuka, sauti zenye lengo la kukufanya unyamaze. Nakupa wewe sauti mwaka huu, sauti ambayo itafanya sauti nyingine zozote za uovu kunyamaza. Kwa wewe nitaliponya taifa. Kwa wewe nitarejesha tumaini pasipo na matumaini. Watu walio waaminifu, hao nitawainua kutoka miongoni mwenu. Watu walio waaminifu, watu ambao huweza kuaminiwa: wataaminiwa kwa ajili ya karama na vipawa; wataaminiwa katika fedha na mali; wataaminiwa kwa thamani ya roho za watu wangu. Kwa wewe mataifa wakaimbe wimbo wa Bwana Mungu wa utukufu aketiye mahala pa kiti chake cha enzi.

Kwa wewe, yule muovu shetani, hatoweza kujitukuza tena juu ya watu wangu, watu nilio waumba nikawaokoa kwa ajili ya jina langu mwenyewe. Nimekuchagua kwa ajili ya shauri langu, nimekuita kwa ajili ya kusudi langu. Kamwe, usiende kando, kamwe usiondoke katika agenda ya yale niliyokuita kwayo; baki katika magoti ya maombi yako. Baki katika magoti ya maombi yako upate kuona na kujua habari ya yale nitakayokuelekeza, sawasawa na muundo wa yote niliyo yapanga kwa ajili yako kutokea mahala pa kiti changu cha enzi.

Kwa ajili yako wewe, wewe kibinafsi, enenda katika njia ya unyoofu, enenda katika njia ya utakatifu; enenda katika njia ya unyoofu, enenda katika njia ya utakatifu. Imwagilie bustani ya maisha yako kwa shukrani za kudumu. Usiruhusu jambo lolote kuiiba shukrani yako kwa Mungu.  Imwagilie bustani ya maisha yako kwa shukrani za kudumu. Imwagilie bustani ya maisha yako maana sitaruhusu magonjwa wala maradhi kukuibia muda wa furaha na shangwe ambao ungeutumia katika kuleta utukufu wa jina langu. Usiutafute msaada wa Misri, usitafute msaada wa miungu maana Mungu huyu unayemtafuta hekaluni mwake ataonekana kwako mapema, ataonekana kwako kwa hakika.

Baki ukiwa mwaminifu, baki ukiwa mwaminifu, baki ukiwa mwaminifu. Mtumikie Yeye kwa furaha, mtumikie Yeye kwa moyo wa kuchangamka maana Bwana atafungua mlango, atafungua mlango, ule mlango wa kifedha unaongojea, ule mlango wa ndoa unaongojea, ule mlango wa kihuduma unaongojea, ule mlango wa nguvu na mlango wa uweza na mlango wa utukufu uko tayari kufunguka. Mlango wa rehema na neema utafunguliwa; mlango wa fursa zilizo mpya utafunguliwa; mlango wa kuinuliwa, kuinuliwa kutakakokufanya uimbe wimbo mpya na wimbo wako ukawe wimbo wa wengi, utafunguliwa. Mlango wa kushangazwa kwa uzuri utafunguliwa. Mlango wa mbingu wenyewe, utakao kunyeshea wewe ile mvua iliyo nzuri, mvua ya Mungu, utafunguliwa kwa ajili yako.

Atapigana vita yako, atawanyamazisha adui zako. Yeye Bwana atalifanya jina lake kujulikana kwa kila farao aliyekuandama. Anaondoa kukataliwa kwako. Anaondoa namna yoyote ya manukato ya uovu juu yako. Anaondoa kila namna ya vazi la mabaya. Atakuzingira kwa wigo wa moto wake. Mungu, huyu Mungu ainukae kwa utukufu mahala pa kiti chake cha enzi atakuficha chini ya mbawa zake ili akufungulie hazina zake nzuri, hazina zile za sirini. Nitakuelekeza, nitakuelekeza kwa sauti ya Neno langu, na katika Mkono wangu wa kuume nikuongoze katika njia yangu. Nitaondolea mbali yote ya fedheha, ya huzuni, kutoka juu yako. Nitakupa yale yote yaliyo mafungamano yaliyo sahihi na ya mkono wa wasaidizi walio sahihi. Mimi Mungu nitakuwa chanzo cha mema yote yanayo kuhusu. Mimi nitakuwa mpaji wako. – asema BWANA.